Loading...
 

Tathmini za Ufanisi

 

 

Tathmini za Ufanisi

Alexander Hristov

 

Kama ambavyo umeona, majukumu mengi yanahusiana na kutathmini wengine. Ni muhimu kutambua kuwa "kutathmini" inamaanisha "kutoa maoni ya kujenga" ili mtu ambaye anatathminiwa aweze kujiendeleza kwa njia maalum. Utathmini haimaanishi kuhukumu au kukosoa watu wengine. 

Jukumu la Mtathmini wa Hotuba ni moja ya jukumu la muhimu sana ndani ya Agora. Utakuwa unampa mwanachama mwenzako utambuzi wa lazima ambao utamsaidia kwenye njia yake ya kielimu. 

Kila mtu anafuzu kuwa Mtathmini wa Hotuba.

 


Bosco Montero, akitathmini hotuba kwenye mkutano wa Agora Speakers Madrid
Bosco Montero, akitathmini hotuba kwenye mkutano wa Agora Speakers Madrid

Swali moja ambalo Watathmini wa Hotuba huuliza ni, "Je, nina uzoefu wa kutosha wa kuwa Mtathmini wa Lugha?" au "Nimefanya miradi michache tu, je, nina uwezo wa kuwa Mtathmini wa Hotuba kwenye miradi ya juu?"

Kwa kawaida, wanadhani, kwasababu hawajafanya hotuba za kutosha, wanakuwa hawana ujuzi au hawana uwezo wa kuwa jaji wa hotuba ya mtu mwingine. 

Hii, lakini, si kweli. Chukulia, kwa mfano, mara ya mwisho umeenda kuangalia filamu na rafiki yako. Je, ulikuwa na maoni kuhusu filamu au uigizaji baada ya kutoka mahala pale? Nina uhakika mambo ya kwanza uliyoyasema kwa rafiki yako baada ya filamu kuisha ni, "Dah, ile filamu ilikuwa nzuri sana. Nilipenda pale ...." au "Mmh, ile filamu ilikuwa mbaya sana. Uigizaji wake ulikuwa mbaya sana". Na hapo, wewe sio mtaalam wa kutengeneza filamu au mwandishi wa filamu, au muigizaji. 

Hii pia ipo katika sehemu mbalimbali za maisha yetu- tunaenda kwenye mgahawa, na tunakuwa na maoni ya chakula hata kama hatujui kupika yai moja tu la kukaanga bila kuchafua jiko zima. Tunaenda kuangalia mchezo kwenye ukumbi, na tunakuwa na maoni kuhusu hadithi na uigizaji, hata kama hatujaenda shule ya sanaa. Tunaenda kuangalia mechi ya mpira, na tunakuwa na maoni ya jinsi kila mchezaji alivyocheza hata kama hatufanyi michezo yoyote ya spoti. 

Sababu ya yote haya ni kuwa hatutathmini kwa mtazamo wa kitaalam.

Lengo la Mtathmini wa Hotuba sio kumtathmini msemaji kwa mtazamo wenye vigezo vya kielimu au kitaalam.

Lengo la Mtathmini wa Hotuba ni kutoa maoni kwa msemaji na kuhusu hotuba kwa mtazamo wako kama mshiriki wa hadhira.  

Kama mshiriki wa hadhira, unajua nini ambacho umekiona, nini ambacho umekisikia, na hisia gani hotuba imekupa. Na umepitia maisha yako yote ukisikiliza hotuba zenye maudhui mengi tofauti. 

Kumbuka pia kwamba, kama Mtathmini, utakuwa unaelezea tu maoni yako. 

Malengo Yako kama Mtathmini

Una malengo matatu ya msingi kama Mtathmini wa Hotuba.

  • Kumpa motisha msemaji. Wasemaji wote ni binadamu, na wote wana mashaka sawa na hitaji la kukubalika kama binadamu wote. Hata kama msemaji ana kiwango cha juu na anaonesha kujiamini, bado atakuwa na mashaka na uoga kwa ndani - "Je, nilifanya kwa usahihi?", "Nilikuwa na ushawishi?", "Hawa watu walinifikiriaje?", "Je, waligundua kuwa nilifanya kosa hili na lile?".  Tofauti pekee kati ya msemaji mwenye kiwango cha juu na mpya kwenye suala la uoga ni namna gani wanadhibiti na kukabiliana nalo. Kwahiyo wasemaji wote watathamini kutambuliwa na kuhimizwa kwa kuambiwa ni vitu gani walifanya kwa usahihi. 
  • Kumuelimisha msemaji na hadhira. Kama Mtathmini, unahitaji kuonyesha ni kitu gani kinaweza kuboreshwa na kwanini  vitu hivyo ni muhimu. Usiseme tu "Ningetumia utofauti wa sauti zaidi". Elezea kwanini utofauti wa sauti ni muhimu kwa ujumla na kwa mradi huu maalum. Maelezo ni kwa ajili ya msemaji, lakini pia kuelemisha hadhira, sababu moja ya njia kuu za kujifunza ni kwa kutazama wengine wanafanya nini.
  • Kumsaidia spika aendelee vizuri zaidi. Wasemaji wote wanataka kupata mwendeleo mzuri, hata zaidi, wale wa juu pia. La sivyo, wangekuwa wanatoza pesa kwaajili ya kuongea kwenye mikutano na sio kuhudhuria klabu! Kumsaidia msemaji aendelee vizuri, inabidi umpe ushauri maalum na ambao anaweza kuufanyia kazi: vitu ambavyo - kwa maoni yako - angeweza kufanya vizuri zaidi au kitofauti ili aweze kuboresha hotuba yake kiufanisi. 

Sasa, sipendekezi kuwa unatakiwa kukumbuka malengo haya, lakini, kama inasaidia, endelea nayo. 

 

Nini cha kufanya kama Mtathmini - Kabla ya Mkutano

Ili kupata ufanisi kama Mtathmini, unahitaji kujua ni nani atakayetoa hotuba na mradi wenyewe. Hata kama "umejitolea" jukumu la kuwa Mtathmini kwenye mkutano, lazima kuna muda kabla mkutano haujaanza wa kujaribu kufanya hatua zifuatazo. 

 

1. Soma kuhusu Mradi 

Soma maelezo ya mradi ambao msemaji atatoa kwa ukamilifu. Weka umakini maalum kwenye malengo ya kujifunza na dhumuni kuu. Haya ndio mambo makuu ambayo msemaji anatakiwa kuyapata kutoka kwenye mradi.

 

2. Pambanua Muktadha

Tathmini zote zinatakiwa kuwa maalum kwa muktadha wa kile kinachotokea. Muktadha unajumuisha vitu kama:

  • Madhumuni ya Mradi 
  • Malengo kwa ujumla ya njia ya kielimu ambayo msemaji anafuata
  • Kiwango cha msemaji 
  • Ni vitu gani maalum msemaji anapendelea
  • Mahali
  • Muda
  • Matukio Yaliyopita na Yanayofuata

Mfano wa jinsi muktadha unavyoshawishi utathmini mzuri, ni kuzingatia kiwango cha msemaji. Wakati mtu anaanza usemaji wa umma, maoni kwenye vitu vya kawaida kama kuwatazama hadhira vizuri machoni yanaweza kuelezwa mara nyingi na kwa urefu. Kwa mfano, "Wakati wa hotuba yako, haukuangalia sana upande wa kushoto wa hadhira. Kuwatizama vizuri washiriki wote machoni ni muhimu kwasababu nyingi - mara moja inamvutia mtu ambaye unamtazama kuwa makini, unaonesha kujiamini na kuwa na mamlaka, na unatengeneza mazingira ya kirafiki ya maongezi ya moja kwa moja na mtu huyo".

Kama msemaji angekuwa ni mwenye ujuzi wa miradi 20, maelezo ya juu yasingekuwa muhimu na yangepoteza muda muhimu ambao bora ungetumika kutoa maelezo kwa vitu ambavyo msemaji havijui. Tambua kuwa hii haimaanishi kwamba usivitaje kabisa. Tofauti kabisa, wasemaji wote - hata ambao ni wa kiwango cha juu - wanafanya makosa ya kawaida mara kwa mara. Kwahiyo sema kitu kama, "Wakati wa hotuba yako, haukuangalia upande wa kushoto wa hadhira.", lakini usiliwekee msisitizo - msemaji wa kiwango cha juu tayari analifahamu hilo. 

Pia, wasemaji wenye uzoefu wanapenda kupata maoni zaidi ya jinsi ya kujiendeleza, lakini wasemaji wapya wanahitaji zaidi kuhimizwa na vidokezi vichache vya kujiendeleza kadri muda unavyokwenda. 

Ukumbi pia ni muktadha muhimu. Msemaji mzuri anahitaji kubadilika ili aweze kuhimili kumbi mbaya:

  • Jiometri - Mara nyingine, ukumbi ni mbaya kwasababu hadhira haijakaa kwenye sehemu moja lakini wametawanyika katika maumbo mbalimbali. Wasemaji wazuri watahakikisha wanalifanyia kazi hili na kuwatazama machoni hadhira yote bila kujali wamekaa wapi. 
  • Mazingira sikizi - Kumbi zingine zina mazingira sikizi mabaya sana, na msemaji mzuri lazima afidie hilo kwa kupaza sauti zaidi.
  • Mwanga - Mara nyingine, taa zina mwanga hafifu sana, na msemaji lazima atumie msisitizo zaidi ili kuepusha watu kulala. Mara nyingine taa zina mwanga mkali sana, ambayo inaweza kuleta tatizo kama msemaji anatumia vielelezo vya kuona au vifaa vya projekta.
  • Halijoto - Kama ukumbi hauna halijoto, unyevu, au upitishaji wa hewa unaofaa, watu watakuwa makini na karaha inayowapata, kitu ambacho kitamlazimu msemaji kutumia nguvu ya ziada kumudu umakini wao. Msemaji mzuri mara nyingine anaweza akajumuisha suala lile kwa njia inayofaa (kwa kawaida ni kutumia vichekesho) na hapohapo atakamata umakinifu wa hadhira na kuwapa mwelekeo mzuri bila kutumia nguvu kabisa. 

Siku na muda pia ni vitu muhimu sana kwenye hotuba, japokuwa, kwenye mipangilio ya klabu, kuna vitu ambavyo havibadiliki kwasababu klabu nyingi zinakutana kwenye muda uliopangwa katika siku moja ya wiki. Hata hivyo, kwa miradi ya nje ya klabu na duniani kwa kawaida, hotuba inayowasilishwa Jumatatu asubuhi na mapema haipo sawa na hotuba inayowasilishwa Ijumaa kabla ya siku ya kazi kuisha na akili na mioyo ya watu tayari ipo mbali na ukumbi ambapo hotuba inatolewa. Hotuba ya saa 2 asubuhi haitakiwi kuwa sawa na hotuba inayotolewa kabla au baada ya chakula cha mchana. 

 

3. Wasiliana na Msemaji 

Kazi yako kama Mtathmini inaanza kabla hata ya mkutano. Wasemaji wengi wana malengo yao ya ziada kwa kila mradi. Wasemaji wengi wanataka kuhakikisha kuwa wamejifunza na wamefanyia kazi vitu maalum kutoka miradi iliyopita. Ina manufaa kuwa na mtu ambaye atawaonesha ni kwa namna gani wamefanikiwa (au la) wakati wanafanya hivyo. Labda msemaji ana tabia ya kuangalia sana upande wa kushoto wa hadhira? Labda msemaji ana tabia ya kusogea mbele na nyuma muda wote? Labda msemaji anataka kuhakikisha anatamka kwa usahihi? Kuwa anasikika nyuma ya chumba?

Kwa sababu hizo, wasiliana na msemaji kabla ya mkutano na muulize kama anataka uwe makini na kitu chochote maalum, cha kujumuisha na malengo ya mradi. 

 

4. Andika kabla utathmini wako 

Ingawa bado haujasikiliza hotuba bado, unaweza ukaamua mbinu yako ya utathmini kabla ya mkutano na ukaandika kabla muundo wake. Kwa mfano, unaweza ukaamua kabla kwamba unaweza kufungua kwa maoni chanya ya jinsi unavyokumbuka mwanzo wa msemaji mahsusi. Au unaweza kuamua kuanza na uzoefu wako binafsi wa mradi ule. Mwanachama mmoja alikuwa anaanza kila moja ya tathmini zake na "Hotuba yako imenikumbusha.... ", alafu ataendelea na hadithi binafsi. 

Unaweza pia ukachagua baadhi ya nukuu ambazo zinaweza kutumika katika mradi huu mahsusi. Kwa mfano, mradi wa  "Maendeleo ya Hotuba," ambapo lengo kuu ni utumiaji fanisi wa lugha wakati wa uandishi wa hotuba, napenda kujumuisha nukuu ifuatayo kutoka kwa Antoine de Saint-Exupery:

"Kama unataka kujenga meli, hauwalazimishi watu kukusanya mbao au kuwapa majukumuu au kazi, bali unawafundisha kutamani ukubwa wa bahari ambao hauna mwisho."

Nukuu hii inasaidia kuonesha uhitaji wa kutumia lugha ili kupeleka picha imara na hisia kwa hadhira. 

Kumbuka kuwa Utathmini ni pia hotuba yenyewe, na inatakiwa kuwa na vigezo vyote vya hotuba nzuri - muundo, ujumbe, uwazi, mwendo, nk. 

Unaweza ukaandika kabla ni vitu gani vikuu ambavyo unataka kuvizingatia, au labda andika kabla baadhi ya maneno ya msingi ambayo baadae utayapigia mstari au kuyakata (wengine wanapendelea kuandika alama za "chanya" au "hasi") kulingana na jinsi msemaji alivyofanya. Kitu chochote ambacho kitaokoa muda wewe kuandika ulichokiona wakati wa hotuba yenyewe kinakubaliwa, kwani kitakupa muda zaidi wa kuwa makini na hotuba. 

Nini cha kufanya kama Mtathmini - Wakati wa Mkutano 

 

Wapi kwa Kukaa

Unatakiwa ukae sehemu ya kutokuwamo, isiyo na upendeleo. Usipate kishawishi cha kukaa mstari wa mbele ili "uone na usikie" msemaje dhahiri, kwasababu hivyo sivyo hadhira, kwa ujumla, watakavyochukulia. Kumbuka kuwa kama Mtathmini, wewe sio jaji rasmi wa utendaji ambaye maoni yake ni muhimu kuliko ya mtu mwingine yoyote, lakini ni mshiriki tu wa hadhira ambaye umekubaliwa kutoa maoni yako kwa umma kwenye utathmini wa hotuba ndogo. 

 

Sikiliza kwa Umakini 

Ni wazi kwamba ili kutathmini hotuba, inabidi usikilize kwanza, na usikilize kwa umakini sana. Natumai, kwa sasa, umeshaandika kabla vitu ambavyo utavitilia mkazo, ili usipoteze muda kuandika. Sahau kuhusu kinywaji chako, chakula chako, simu yako, watu wa pembeni yako kwenye hadhira, au mshiriki ambaye unaanza kumpenda... Sahau kila kitu kingine.  

 

Chukua muhtasari

Haijalishi unafikiri kumbukumbu yako ni nzuri kiasi gani, sio nzuri kihivyo. Usijidanganye kufikiria kuwa utakumbuka hiki na kile kuhusu hotuba - iandike.  Hasa, andika, inavyotokea: 

  • Semi na sentensi maalum ambazo umeziona ni za kipekee kwa uzuri au kukumbukwa
  • Ishara au mienendo yoyote ya mwili ambayo ilifaa kufikisha ujumbe mkuu (au ambao, kwa kinyume, haikuwa sawa, ilikuzwa sana, au haikufaa pale) 
  • Vielelezo vya kuona au vitu ambavyo vilikuwa tofauti kabisa au ambavyo havikutumiwa kwa mafanikio. 
  • Kwa ujumla, sehemu yoyote ya uwasilishi wote ambao ulikuwa mzuri (au kinyume). 

 

Wakati unachukua muhtasari, hakikisha unaandika kwa namna ambayo itakuwa rahisi kuisoma tena! Zaidi ya mtathmini mmoja au wawili wameteseka kwenye jukwaa kwasababu hawakuweza kusoma miandiko yao wenyewe.

Pendekezo zuri ni pia kuandika kwa herufi kubwa. Hii itakuwezesha kusoma kirahisi, kuondoa muhtasari, na usivishike mikononi. Utaweza kuviweka kwenye mimbari au kiti kwenye mstari wa kwanza na kusoma kwa mbali. 

Wakati unachukua muhtasari, amua pia umuhimu wa kila suala ambalo umeliandika. Hautokuwa na muda, wakati wa utathmini wako, kusema kila kitu kimoja kimoja. Kwahiyo ni njia nzuri ya kuweka namba muhimu kwa kila mtazamo (baadhi ya watu hutumia "+","++", na "+++" kwa mfano, sawa na "-" kwa pointi za nini cha kuboresha), na alafu huandika kwa haraka ufupisho wa nini cha kusema hotuba ikiisha. 

 

Onyesha unajali

Hata kama hawatakiwi, wasemaji wanamuangalia kwa uangalifu zaidi mtathmini kuliko watu wengine kwenye hadhira. Mpaka wakati ambao, inaonekana kawaida na sio tatizo. Lakini hii inaweka jukumu zaidi kwako. Unatakiwa kuonesha unajali kuhusu hotuba kwa kumtazama zaidi machoni, viashiria vidogo kukubali kama vile kutikisa kichwa, kuunga mkono pale inapohitajika- kwa mfano, msemaji akisema kitu cha utani au kisa cha kuchekesha.

 

Vitu ambavyo havihusiani na utathmini

Wakati unasikiliza hotuba, daima ni vizuri kukumbuka si tu vitu ambavyo vitatathminiwa bali pia ambavyo havitathminiwi:

  • Chaguo la maudhui kwa kawaida halitathminiwi, isipokuwa kusema ni kwa namna gani inafanikisha malengo ya mradi. Kwa mfano, kwa mradi unahusu Lugha ya Mwili, basi unaweza kutoa maoni kama chaguo la mada lilileta fursa kwenye hilo au la. Zaidi ya hapo, wasemaji wana uhuru wa kuchagua mada ambayo wanataka kuongelea. 

 

  • Maudhui kwa kawaida hayatathminiwi, isipokuwa kwenye miradi fulani michache sana. Hata kama haukubaliani na maudhui, jaribu kutokutoa maoni kwenye hilo, au kubishana na msemaji au kuanzisha mdahalo wa nani yupo sawa au amekosea.

 

  • Mtu kamwe hatathminiwi. Usitoe maoni kuhusu mavazi ya mtu, au mtindo wako, au chaguo lake la mavazi ya nyongeza au mapambo, isipokuwa kama inaathiri hotuba kwa njia maalum. Kwa mfano, kama msemaji amevaa bangili na zinatoa sauti ya usumbufu kila mara akisogeza mkono wake, hilo linaweza likasemwa. Lakini, kutoa maoni kama "Leo umevaa gauni nzuri sana" au "hiyo ni suti nzuri umevaa leo" haifai kabisa.

 

Nini cha kufanya kama Mtathmini -  Tathmini yenyewe 

Kwa kawaida, mtazamo uliopendekezwa wa kuwasilisha Utathmini wa Hotuba unaitwa mtazamo wa "sandwichi", unaoambatanisha safu moja ya maoni chanya na vitu ambavyo ulivipenda, alafu safu nyingine ya vitu vya kuboreshwa, alafu safu moja ya kuhitimisha vitu ambavyo ulivipenda. Sandwichi inaweza ikawa na urefu wa safu kadhaa kama ukirudia mpangilio huu. 

Sandwich Approach Blank
maoni chanya 
pointi za kuboresha
maoni chanya 

Ni namna gani "unene" wa kila safu unavyotakiwa kuwa? Hii inategemea sana na kiwango na kujiamini cha msemaji.

  • Kwa wasemaji wanaoanza, 40% iwe chanya, 20% ya nini cha kuboresha, 40% ya kuhimiza. Hii inamaanisha kwenye utathmini, utaelezea tu pointi chache za nini cha kuboresha, pointi kuu.
  • Ila, kwa wasemaji ambao wana kiwango cha juu huwa wanapendelea 20% 50% 30%, ikimaanisha pointi tano au sita za nini cha kuboresha na pointi mbili au tatu imara ambazo ni chanya.  

 

Uwasilishi wa Maoni Chanya 

Kwa kawaida, maoni chanya ni sehemu rahisi sana. Ila, ni rahisi sana kuingia kwenye mitego hii michache:

  • Sifa - Sifa ni kitu chanya kabisa, na kila mtu anapenda kupokea sifa, lakini sifa sio maoni. Tofauti ni kuwa sifa sio mahsusi, na msemaji hawezi kujua ni kitu gani maalum ambacho alifanya kilichompatia sifa ile, ili aweze kukirudia au kukijenga. Kwa mfano, "Kazi nzuri sana kwenye hadithi. Kazi nzuri sana!" - hii ni sifa tu ambayo sio mahsusi. Ila, kama ukisema, "Kazi nzuri sana kwenye hadithi. Nimependa wasifu wa msichana na jinsi ulivyoelezea kwa kina wasifu wake, na pia jinsi ulivyoiga sauti yake", basi hayo ni maoni chanya. Jitahidi kuepuka vivumishi vinavyotumiwa sana ambavyo havina maana sana "utofauti wa sauti mzuri", "hotuba nzuri", "uwasilishi bora sana", isipokuwa kama yanafuatwa hapo hapo na maelezo ya kwanini ulifikiria hivyo. 

 

  • Vitu visivyo na maana - Usiingie kwenye mtego wa kutoa maoni chanya au - mbaya zaidi, au hata, sifa - kwenye vitu visivyo na maana. Hii ni haswa kwa wasemaji wa kiwango cha juu. Kwa wanaoanza, ni vizuri na inawahimiza ukisema kuwa hakutumia vidokezo au alikuwa anatazama watu machoni vizuri sana na hata kutoa maoni kuhusu wao. Lakini, kwa msemaji wa kiwango cha juu, hivi vitu vinakuwa tayari havina maana. Ukijaribu kuvaa viatu vya mtu ambaye tayari ameshawasilisha miradi 20+, na anasikia kwa mara ya 21, "Haukutumia muhtasari, ilikuwa vizuri sana...
     
  • Maoni chanya mengi sana.  Uwingi wa kitu unaweza kuwa mbaya. Wanachama wote wa Agora wanajiunga kujiendeleza na kujifunza. Kama Utathmini una 80% (au mbaya zaidi, 100%) maoni chanya, wanachama anaweza kufikiri, "Sawa, kama mimi ni msemaji mzuri sana, kwanini nipo hapa sasa?" 

 

  • Maoni chanya kama sababu au ishara mchanganyiko. Watu mara nyingi wanatumia maoni chanya kama sababu au kupunguza makali ya kinachofuata. Unaweza ukaona kama kitu cha kujengea kwa mfano "Nimependa ..... LAKINI .... ". Hiyo LAKINI inaweza ikafuta kila kitu ambacho kilisemwa kabla na inafanya utambulisho kutokuwa na maana ukilinganisha na tamko la ukweli ambalo lilifuata. Jiepushe na hili. Maoni chanya yanatakiwa kusimama yenyewe. 

 

Uwasilishaji wa Maoni Kwa ajili ya Kujiendeleza

Kwa kawaida, uwasilishaji wa sehemu hii ni mgumu sana. Sababu za ugumu huu zinaweza kuwa: 

  • Hatutaki kuwa wakosoaji 
  • Hatuna uhakika na uzoefu wetu wenyewe 
  • Hatuna uhakika na ujuzi wetu wenyewe
  • Hatuna uhakika kama tumesikia au tumeona kwa usahihi.

Ili kuyashughulikia, kumbuka kuwa hautoi alama kwa msemaji lakini unaelezea maoni yako na kutoa ushauri wako ni namna anaweza kujiendeleza. 

Ili kuwa na faida, pointi za maendeleo lazima ziwe: 

  • Zinazotoa pointi mahsusi. Tena, hii ndio ambayo inatofautisha ukosoaji na maoni. Ukosoaji, kama sifa, haina mahsusi maalum na mara nyingi inakuwa kibinafsi. "Utumiaji wako wa lugha ya mwili ni mwingi sana" ni mfano wa ukosoaji. Lakini, ukisema badala yake, "Ulivyoruka kwenye meza, na kuanza kuigiza kama sokwe, na ukajining'iniza kutoka kwenye taa, nafikiri pale ulionesha sana lugha ya mwili.
     
  • Zinatoa mwongozo. Hii inamaanisha sio tu kwenye pointi mahsusi ni usehemu gani ya uwasilishi inaweza ikaboreshwa, lakini pia unatoa ushauri wa jinsi wanaweza kujiboresha. Tukiendelea na mfano uliopita, unaweza ukaongeza kuwa, "Nafikiri kuweka mikono yako na kujikunja kama sokwe wanavyojikunja na kutembea hatua chache kama hivi kulitosha kuwasilisha pointi". 
     
  • Zinazoweza kufanyiwa kazi. Hii inamaanisha kuwa mtu anaweza kweli akafanya kitu kuhusu kitu ambacho haukukipenda. Kwa mfano, kama mtu ana sauti kali au ya kukwaruza, basi hiyo ndio sauti aliyokuwa nayo. Sio maoni ya kujenga kabisa kumwambia, "Ningependa kupendekeza kuwa ukiwa unasoma mashairi ya mapenzi utumie sauti tofauti, nyororo na ya kimelodia zaidi."·

Ikifika kwenye kuwasilisha pointi za maendeleo: 

  • Usirudie mapendekezo. Inatosha ukielezea mara moja, hamna haja ya kuzirudia mara kwa mara. 
  • Usitumie lugha ya kuamuru. Wewe sio bosi wa msemaji. Jaribu kuepuka "Unatakiwa", "Unahitaji" (au, isiyopendwa "lazima"), au kwa ujumla, lugha ya "kunyooshea kidole". Badala yake, njia iliyopendekezwa ni kusema "Ningefanya hivi na hivi badala yake", "Ningependekeza kuwa ufanye kwa njia hii", "Ningependekeza kuwa u..", "Ningetoa", nk.
  • Usiongee kwa ukamili. Kumbuka kuwa wewe unatoa tu maoni yako, na sio ukweli wa ulimwengu. "Utofauti wa sauti ulikuwa na kasoro". Badala yake, elezea kuwa "Sikutambua utofauti mwingi wa sauti - Nakumbuka mifano mitatu, ulivyoiga ya msichana mdogo, mbwa mwitu na bibi kizee."
  • Usiongee kwa niaba ya wengine. Tena, hii inahusiana na pointi iliyopita. Hauhitaji kuthibitisha chochote kwa msemaji au hadhira. Kwa mfano: "Nadhani wote tunaweza kukubali kuwa lugha ya mwili inaweza ikaboreshwa". 
  • Na mwisho, elezea kile ambacho umekiona badala ya ulichodhania kuhusu sababu za msingi. Kwa mfano, usiseme, "Nahisi hotuba haikuandaliwa vizuri," kwasababu huna uthibitisho wowote ule wa udhanifu huo. Badala yake, unaweza kuelezea kwa uhalisi ulivyohisi: "Nilihisi kuna wakati ulisita au haukuwa na uhakika wa nini cha kusema baada."  

 

Hitimisho La Utathmini 

Hitimisho la Utathmini linatakiwa kutoa tena kwa ufupi pointi chanya, pointi za kufanyiwa maboresho, na kumaliza kwa neno la motisha na la kuhimiza. 

Jaribu kuepuka kutumia maneno au sentensi zinazotumiwa sana, hasa, "Nangojea hotuba yako inayofuata". Jaribu kuwa mbunifu. Panga hitimisho kabla hata hotuba haijaisha. 

 

Nini cha kufanya kama Mtathmini - Baada ya Mkutano

Baada ya mkutano, ongea na mtu uliyemtathmini ili uone kama ana mashaka au maswali yoyote.  

Pia, kumbuka kujaza kadi ya utathmini ya mradi huo. 

 

Jinsi ya kuwa Mtathmini mzuri 

Siku zote, mazoezi huleta ufanisi. Lakini hauhitaji kuwa mtathmini kupata mazoezi. Kwa mfano, unaweza kufanya hatua zote ambazo mtathmini anahitaji kufanya bila kuwasilisha kwa umma. Na ni vizuri kujifunza kwa kujilinganisha utathmini wako na ule utakaotolewa na Mtathmini wa mkutano.

 

Ukiwa wewe ndio unayetathminiwa 

 

Ukiwa wewe ndio unayetathminiwa, kubali utathmini kwa upole na kama zawadi. Mtathmini anakusaidia uendelee. Usichukulie chochote kibinafsi.

Usijibizane na Mtathmini, hasa wakati wa utathmini wenyewe - yeye anaelezea maoni yake na kukuambia jinsi ambavyo aliona na kuhisi wakati wa uwasilishi wako. 

Kama ungependa kutoa maelezo au kujadiliana kitu na yeye, fanya hivyo baada ya mkutano. 

 

Wakati gani wa KUTOKUWA Mtathmini

Pale utakapokuwa Mtathmini hai na anayethaminiwa kwenye klabu, utatamani kutumia ujuzi wako sehemu nyingine. Fanya hivyo kwa tahadhari, ikiwezekana. Wasemaji wa klabu wanakuja na lengo la kutathmini na kupewa maoni; wanategemea, na wanathamini maoni hayo. Hili sio suala la watu wote au wasemaji wachache kwenye matukio mengine. 

Fikiria upo kwenye sherehe ya utoaji tuzo, alafu unamfuata mshindi baada ya sherehe na kumwabia kitu kama, "Nilipenda hotuba yako ya kupokea tuzo. Nilipenda jinsi ulivyopaza sauti yako mpaka nyuma ya chumba ili kila mtu aweze kukusikia. Naweza kupendekeza kuwa uangalie hadhira yako machoni kwa uendelevu? Niliona kuwa uliangalia sana upande wa kulia wa chumba, na ...

Unaweza kuona ni kichekesho, lakini inatokea. 

Kuna tofauti kati ya kuwa mwalimu ukiombwa na kutoa maoni na kufundisha ulimwengu kwa ujumla. 

 

 


Contributors to this page: agora and zahra.ak .
Page last modified on Monday August 30, 2021 01:43:31 CEST by agora.